.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 20 Aprili 2014

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR MAALIM SEIF AHIMIZA UPANDAJI WA MITI


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipanda mti katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipanda mti katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Affan Othman Maalim (kushoto) katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, barabara ya Jendele/Unguja Ukuu


Baadhi ya wananchi wakishuhudia uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR). 

Jamii imehimizwa kukitumia kipindi hiki cha mvua za masika kupanda miti kwa wingi, ili kurejesha hadhi ya Zanzibar ya kuwa “Visiwa vya Kijani”.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akizindua zoezi la upandaji miti Kitaifa katika barabara ya Jendele Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kwa kiasi kikubwa jamii imepoteza utamaduni wa asili wa kupanda na kutunza miti, hali inayopelekea kutoweka kwa baadhi ya miti mikubwa ya matunda na viongo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Hivyo ameziagiza serikali za Mikoa na Wilaya kusimamia utunzaji wa miti inayopandwa, ili kuhakikisha kwamba inakuwa vizuri na kuleta ustawi uliokusudiwa katika utunzaji wa mazingira na kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema miti ina umuhimu katika uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji vikiwemo chemchem na mito, pamoja nakujikinga na upepo mkali, sambamba na kusaidia upatikanani wa mvua ambayo ni muhimu kwa shughuli za kilimo na ustawi wa maisha ya binaadamu na wanyama.
Ameongeza kuwa miti ni chanzo kikubwa cha pato la wananchi na Taifa kwa jumla, akitolea mfano zao la karafuu ambalo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa Zanzibar.
Maalim Seif ametumia fursa hiyo kukemea tabia ya baadhi ya watu kusafirisha miche ya mikarafuu nje ya nchi, pamoja na kuacha kabisa matumizi ya misumeno ya moto ambayo ni adui wa mazingira.
“Nakuombeni wananchi tupande kwa wingi mikarafuu na miti ya matunda pamoja na viungo, ili kuiweka nchi yatu katika haiba nzuri ya kupendeza ambayo inaweza kuwavutia hata wageni wetu”, alisema Maalim Seif na kuongeza,
“Lengo la Serikali ni kupanda miti katika barabara zote Unguja na Pemba, hivyo nakuombeni sana wananchi tushirikiane ili kufanikisha lengo hili”.
Kwa upande mwengine Maalim Seif amewataka wafugaji kuheshimu juhudi za serikali na wananchi katika kuitunza miti hiyo, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za sensa ya miti zinaonesha kuwaidadi ya miti inapungua kwa kiasi kikubwa ambapo maeneo mengi ya misitu pamoja na mashamba yamegeuzwa kuwa makaazi ya watu na hivyo kuendelea kukatwa kwa kasi.
Takwimu hizo zinaonesha kwamba katika mwaka 1997 visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa na miti yenye mita za ujazo wa 10.3 milioni, lakini kima hicho kilipungua hadi kufikia mita za ujazo 8.6 milioni mwaka 2013.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim, amesema jumla ya miembe 450 imepandwa katika uzinduzi huo wa upandaji wa miti kitaifa, ambapo wanakusudia kuendeleza zoezi hilo katika barabara yote ya Jendele hadi Unguja Ukuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati bw. Vuai Mwinyi amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa zoezi la upandaji miti tayari limefanyika katika Wilaya za Kati na Kusini, na kuahidi kusimamia utunzaji na uendelezaji wa miti hiyo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni