Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape
Nnauye akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Sekretarieti,makao
makuu ya Chama Ofisi Ndogo Lumumba jijini Dar es Salaam.
Na Bashir Nkoromo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea
kwa furaha Chama cha Frelimo kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktoba 15, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, aliyekuwa
mgombea kwa tiketi ya Frelimo, Mhe Filipe Nyusi ameibuka kidedea na
sasa ndiye Rais Mteule wa Msumbiji ambaye baada ya kuapishwa atashika
mikoba itaakayoachwa na Rais anayemaliza muda wake, Armando Gwebuza.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo, katika ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya
CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye (Pichani), amesema, CCM imepokea ushindi huo kwa furaha
kubwa kutokana na undugu wa damu uliopo baina yake na Frelimo kwa
mikaka mingi.
"Chama Cha Mapinduzi
kilifuatilia kwa karibu kwa kuwa CCM na Chama cha Frelimo ni vyama
ndugu vyenye historia moja na ya pamoja ya Ukombozi Kusini mwa
Afrika. Historia hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Mteule wa nchi hiyo
Ndugu Filipe Nyusi mara baada ya kuteuliwa kwake na Frelimo kugombea
Urais, nchi ya kwanza kuitembelea kuwa Tanzania", alisema Nape
na kuongeza;
"Ikumbukwe kwamba huyu si mgeni
hapa Tanzania. Kama wanaharakati wengine wa ukombozi, Ndugu Nyusi
aliishi Tanzania, anaongea vizuri Kiswahili na anaichukulia Tanzania
ni nyumbani".
Alisema kwa mnasaba huo, Chama Cha
Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kushangilia
ushindi walioupata ndugu zao wa Frelimo, kwa kuwa ushindi huo ni wa
wote.
"Tunampongeza sana Rais Mteule
Filipe Nyusi kwa kupeperusha vema bendera ya Frelimo. Matokeo ya
Uchaguzi yamedhihirisha imani kubwa waliyonayo wana-Msumbiji kwa
Frelimo na kwa Rais Mteule Filipe Nyusi", alisema Nape.
Nape amesema CCM ina imani kwamba
chini ya uongozi imara wa Mwenyekiti wake Dk. Jakaya Kikwete, na Rais
Mteule Filipe Nyusi, uhusiano kati ya vyama vya CCM na Frelimo
utaimarika na kustawi.
Kadhalika Chama Cha Mapinduzi
kimempongeza Armando Guebuza kwa kuiongoza Frelimo na Taifa lake
vema na kukamilisha uongozi wake kwa mafanikio makubwa.
"Anapoanza kipindi hiki cha
uongozi wa Taifa lake, sisi wana-CCM tunamtakia Ndugu Nyusi afya
njema, busara, maarifa na uongozi uliotukuka", alisema Nape.
Alisema, CCM itasimama pamoja na
Frelimo katika kuendeleza urithi ulioachwa na waasisi wa vyama vyao,
Mwalimu Julius Nyerere na Samora Machel.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni