.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 25 Februari 2015

PATO LA MWANANCHI MBEYA LAVUKA LENGO LA KITAIFA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameupongeza uongozi wa mkoa wa Mbeya kwa kuvuka lengo la wastani wa pato la mwananchi kitaifa na kuwataka waendeleze kasi ya kupambana na umaskini kwa wakazi wa mkoa huo.

Ametoa pongezi hizo jana usiku (Jumanne, Februari 24, 2015) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo na wilaya zote wakiwemo wadau mbalimbali na viongozi wa dini mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Mbeya.

Alisema katika mipango yake, Serikali ililenga kwamba pato la mtu kwa mwaka liwe sh. 1,186, 200, lakini kwa sababu ya jitihada mbalimbali mkoa huo umelivuka. “Katika taarifa aliyonisomea, Kaimu Mkuu wa Mkoa amesema wastani wa pato la mwananchi umeongezeka kutoka sh. 711,201/- mwaka 2008 hadi kufikia sh 1,420,427/- mwaka 2013 na kwamba mkoa unachangia asilimia 7.43 ya Pato la Taifa,” alisema.

Alisema kipato cha mtu mmoja kwa siku ni sh. 3,891/- ambazo ni zaidi ya Dola mbili za Marekani (sh. 3,400/-). “Wakubwa hawa wanatupima kwa kuangalia kipato cha mtu kwa siku. Wanasema nchi ni maskini iwapo watu wake wanaishi chini ya dola moja kwa siku (sawa na sh. 1,700/-).”

“Mbeya imeendelea kushika nafasi ya tatu kwa kuchangia vizuri Pato la Taifa ikiwa imetanguliwa na Dar es Salaam na Iringa. Ninawapongeza kwa sababu mmevuka malengo ya Taifa katika eneo la pato la mtu mmoja mmoja,” alisema Waziri Mkuu.

Mapema, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Deodatus Kinawilo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, alisema pato la mkoa limeongezeka kutoka sh. trilioni 1.779 mwaka 2008 na kufikia sh. trilioni 3.951 mwaka 2013.

“Uchumi wa mkoa huu unategemea kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvunaji mazao ya maliasili, biashara, uzalishaji viwandani na ajira katika taasisi za serikali na sekta binafsi,” alisema.

Wakati huohuo, uongozi wa mkoa wa Mbeya umetakiwa kuongeza bidii ili uweze kuinua kiwango cha ufaulu wa elimu ya kwa sababu umekuwa ukiendelea kushuka na kuwa chini ya kiwango cha asilimia 60 kilichowekwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliutaka uongozi huo ubuni mbinu za kisomi zitakazowawezesha wanafunzi wa shule za msingi kuelewa wanachofundishwa, hivyo, kufaulu mitihani yao vizuri. ”Ufaulu wenu kwa shule za msingi ni asilimia 46.6, uko chini ya kiwango cha kitaifa cha ufaulu kwa asilimia 13.4. Ni matokeo yasiyoridhisha, fanyeni utaratibu maalum ili yapande,” alisema.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni