.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 28 Mei 2015

BALOZI SEIF ASEMA HAKUMAANISHA KUMUUNGA MKONO MH MEMBE, BALI KUMTAKIA HERI KATIKA SAFARI NGUMU KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015


                                                                                              Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa wana Habari kutumia vyema kalamu zao sambamba na kuzingatia maadili ya jukumu lao la kazi na kuepuka utashi unaoweza kuleta sintafahamu ambayo inaweza kuibua malumbano na hatimae chuki kati yao na Viongozi.

Balozi Seif ametoa nasaha hizo kufuatia Taarifa ya Gazeti moja Nchini lililochapisha Taarifa yenye kichwa cha Habari “ Makamu wa Rais Zanzibar amuunga mkono Membe “ wakati aliufunga Mkutano wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania Nchi mbali mbali Duniani uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Ramada Jijini Dar es salaam.

Balozi Seif akionyesha mshangao na kusikitishwa kwake kutokana na Taarifa hiyo alisema alichokitamka wakati akikaribishwa na Waziri Membe kuufungua Mkutano huo ni kumtakia safari njema Waziri huyo ambayo ni ngumu.

Alisema alichowajibika na ndicho alichokifanya kwenye Mkutano huo ni kumuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuufungua Mkutano huo wa Babalozi na si kuzungumzia siasa ambapo sio mahala pake.

Balozi Seif alifafanua kwamba utashi wa kuandikwa kwamba anamuunga Mkono Waziri Membe una lengo la kutaka kumvuruga kisiasa kutokana na wadhifa wake akiwa Mmoja wa Viongozi wa Juu wa Serikali hapa Nchini.

“ Mimi kazi niliyokwendea pale ni kumuakilisha Bosi wangu Rais wa Zanzibar kuufunga mkutano ule kwa niaba yake. Sasa hili la kusema nitamuunga mkono Waziri membe bega kwa bega nimelitoa wapi na saa ngapi ? Nilimwambia namtakia safari njema lakini nikamuasa aelewe kwamba ni safari ngumu ” . Alifafanua Balozi Seif.

Alisema wajibu na maadili ya Viongozi wakuu ni Kumuunga mkono Mgombea ambaye tayari ameshachaguliwa katika ngazi ya juu ya Chama kwa ajili ya kuingia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu.

Balozi Seif alieleza kuwa hatua hiyo imewekwa ili kuwepusha shari na mgawanyiko baina ya viongozi hao jambo ambao linaweza kusababisha mtafaruku endapo Viongozi hao wataamua kujiingiza katika makundi na ndivyo anavyoamini yeye katika muda wake wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliviomba vyombo vya Habari hasa Wahariri wa Vyombo hivyo kuhakikisha kwamba wataendelea kubeba dhima katika kuwapasha Habari Wananchi endapo watakuwa wakitoa Taarifa zenye muelekeo wa kusababisha vurugu na mgawanyiko baina ya Jamii.

Alisema zipo Nchi zilizoshuhudiwa kuingia katika migogoro ya Kisiasa na Kijamii na hatimae kusababisha maafa na Nakama kutokana na Kalamu wa Waandishi zilivyokuwa zikichochea shari na balaa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni