.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 24 Novemba 2015

WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIMA AFYA ZAO KUELEKEA DESEMBA MOSI, 2015.

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu ambayo inaadhimishwa kwa kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela akiwaonesha waandishi wa Habari Bango lenye Takwimu za Hali ya Maambukizi ya VVU nchini Tanzania.

                                                                   Na Nyakongo Manyama- MAELEZO.
WITO umetolewa kwa wananchi kote nchini kuyatumia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka kupima afya zao ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema Siku ya Ukimwi Duniani nchini itaadhimishwa kwa kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za Utoaji wa Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa VVU katika maeneo mbalimbali kote nchini kupitia vituo vitakavyowekwa, Kufungua kituo cha maarifa cha udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida ambayo ni njia kuu kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za Burundi na Rwanda.

Ameongeza kuwa Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendesha mikutano ya kitaalam kuhusu UKIMWI, Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi, Kupokea tamko litakalotolewa na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Uzinduzi wa taarifa ya tathmini ya Sheria zinazotumika zinazohitaji kurekebishwa zinazozuia malengo ya sifuri 3.

Aidha Tume itapokea taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU duniani itakayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuhusu dunia na mapambano dhidi ya VVU.

Dkt. Fatma amefafanua kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine atazindua Mfuko wa UKIMWI ambao utakuwa chachu ya kupunguza maambukizi ya VVU nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia 5.3 huku mikoa ya nyanda za juu kusini ya Njombe, Iringa na Mbeya ikiongoza kwa kuwa na maambukizi zaidi na mikoa ya Manyara, Tanga na Lindi ikiwa na maambukizi ya chini ya asilimia mbili.

Dkt. Kamwela amesema kuwa maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka 19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono yakiendelea kuwa katika hatari ya kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni