.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 12 Februari 2016

TAARIFA YA KIKAO CHA MASAA 72


Kikao cha Kamati ya Kusimamia na Kuendesha ligi (Kamati ya Masaa 72) kimekutana Jumatano katikati ya wiki kupitia taarifa na ripoti mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu (VPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendeea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini.

                                                                                          Ligi Kuu ya Vodacom

Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumpiga usoni kwa box la dawa Dk. Mganga Kitambi wa Coastal Union wakati akitoa huduma kwa kipa wake katika mechi namba 121 kati ya timu hizo iliyofanyika Januari 30, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Yondani alitenda kosa hilo baada ya kumuomba maji Daktari huyo, lakini akamnyima. Adhabu huyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 ambapo baada ya kutumia adhabu ya mechi hizo, hataruhusiwa kucheza hadi atakapokuwa amelipa faini hiyo.

Naye Dk. Kitambi anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kitendo chake cha kumrudishia Yondani kwa kumpiga ngumi. Kitendo cha Daktari huyo ni kinyume cha Kanuni ya 41(2), na pia Kanuni ya 36 kuhusu mchezo wa kiungwana.

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa Coastal Union walipokuwa wakishangilia bao la pili.

Nayo klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa washabiki wake kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni ya 14(11) inayohusu taratibu za mchezo.

Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia chumba cha waandishi wa habari badala ya kile cha timu wakati wa mechi kati yao na Simba iliyochezwa Februari 3, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Kocha Ally Jangalu wa Coastal Union ameripotiwa kutoa matamashi ya kuidhalilisha TFF kwenye vyombo vya habari kuwa Refa wa mechi kati yao na Ndanda SC iliyochezwa mjini Tanga alikwenda na maelekezo ya kuhakikisha wapinzani wao wanashinda. Coastal Union ilifungwa bao 1-0 katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2016. Suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.


Mchezaji Daud Jumanne amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumkanyaga vidole kwa makusudi mchezaji wa Simba aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Februari 7, 2016 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015. Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 37(20), hauruhusiwi kucheza mechi inayofuata ya timu yake mpaka faini hiyo iwe imelipwa. Iwapo atacheza kabla ya kulipa faini hiyo, timu yake itapoteza mchezo husika.

Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya African Sports iliyochezwa Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) kuhusu taratibu za mchezo.

Kamishna wa mechi hiyo namba 140, Idelfonce Magali amepewa karipio kwa kutoripoti vizuri tukio hilo, wakati Refa Elly Sasii amepewa karipio kali kwa kutoripoti kabisa tukio hilo.

Ligi ya StarTimes

Wachezaji Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Seleman na Edward Amos wa Polisi Dodoma wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kumzonga, kumtolea lugha ya matusi ya nguoni na kutaka kumpiga Refa katika mechi ya Ligi ya StarTimes kati ya timu yao na African Lyon iliyofanyika Januari 30, 2016.

Kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ni kinyume cha Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa wachezaji.

Kiongozi wa Friends Rangers, Heri Mzozo anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kutoa lugha chafu kwa viongozi na waamuzi muda wote wa mchezo dhidi ya Ashanti United uliofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Vitendo vyake ni kiyume na Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.

Mwamuzi Msaidizi namba 2 kwenye mechi kati ya Kimondo na Ruvu Shooting, Idd Mikongoti wa Dar es Salaam ameripotiwa na Kamishna kuondoka na timu ya Ruvu Shooting kwa kupanda basi lao mara baada ya mchezo, kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya uamuzi. Suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi kwa ajili ya hatua stahiki dhidi yake.

Klabu ya Geita Gold imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na onyo kali kwa kukataa kuingia kwenye chumba cha wachezaj, na badala yake kutumia chumba kingine ambacho pia walijisadia haja ndogo wakati wa mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo cha mshabiki wake kupita pembezoni ya uwanja (running track) kwa kasi wakati mechi hiyo dhidi ya Geita Gold ikiendelea.

Pia klabu ya Polisi Tabora imepewa onyo kali kutokana kipa wa timu yake kuvaa jezi ambayo haikuwa na nembo (logo) ya Mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza wakati wa mechi hiyo.

Geita Gold imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya JKT Oljoro kugomea mchezo kati ya timu hizo uliofanyika Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls mkoani Geita. Timu hiyo iligomea mechi hiyo dakika 70 baada ya kufungwa bao la pili. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 29(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Pia JKT Oljoro imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na kitendo hicho kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4), wakati wachezaji wake Kapteni Shaibu Nayopa na Sunday Paul waliomvamia na kumpiga Refa wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki.

Naye Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro, Bunu Abdallah ambaye alitolewa kwenye benchi la timu yake kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba 1 anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua stahiki.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni